Sisi WanaJumuiya wa Tuko Sawa tumeamua kuishi maisha yanayoheshimu Asili na zawadi zake kwetu. Tunashirikiana kwa hali na mali kueneza maadili ya ubinadamu kwa matendo ili vizazi vijavyo wakiuliza tulifanya nini kuhakikisha ustawi wao, tuwe na jibu lenye uadilifu.



Tuko Sawa ni dhana muhimu inayotukumbusha kuhusu usawa wa ubinadamu wetu. Wote tumezaliwa kwenye sayari hii, tutaishi muda kidogo na hatimaye wote tutarudi kwenye mzunguko asilia wa Uumbaji. Ili kuweza kushiriki mzunguko huu kwa UTULIVU, inatubidi kujitambua, sisi ni nani, tunahitaji nini kuishi kwa FURAHA, na je tunaongeza thamani gani kwa jamii? Wanaharmony tunaamini kuwa kila mwanadamu amekuja na zawadi zake duniani hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzitambua ili kutimiza lengo la maisha duniani. Utofauti ni Kanuni asili ya HARMONY.



Jumuiya yetu ni mtandao wa wanaharakati wa Maadili Asilia na Elimu Shirikishi ya Harmony kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania tulioamua kujenga jamii chanya zinazoshirikiana kwa misingi ya UTU-UPENDO-UMOJA bila kujali UTOFAUTI wetu wa ki-dini, ki-umri, ki-kabila au ki-siasa.


"Tuko Sawa" ni msemo unaokiri Usawa katika Umoja wa Uumbaji.


TukoSawa ni dhana yenye manufaa sana katika kujikumbusha kuwa sisi sote tumeumbwa sawa, tumejaliwa kuwa na ufahamu na kwamba tuna uwezo wa kuchagua “kuwatendea wengine kama tunavyopenda sisi kutendewa.” Hii ndio dira ya maadili inayoitwa“Kanuni ya Dhahabu,” ambayo iliongoza tamaduni nyingi za kale na inatajwa kwenye maandishi mengi matakatifu ulimwenguni kote.


Dhana ya Tuko Sawa inapanua kanuni ya dhahabu kwa kuijumuisha Asili kwa uelewa kwamba, kile tunachofanyia Asili tunajifanyia wenyewe. Kutia sumu kwenye udongo au kuchafua maji kunaathiri afya zetu kiujumla kwa sababu chakula chetu hakitakuwa salama. Tuko Sawa ni falsafa ya kiroho inayotuongoza kuwajibika kufanya kitu sahihi hata kama hakuna mtu anatuona. Sisi Mabalozi wa Tuko Sawa tumeamua kuiweka dhana hii kwenye vitendo, ili kutendea haki #UkuuWaUbinadamu wetu.


MAADILI YA MSINGI YA TUKO SAWA NI:

UTU, UPENDO NA UMOJA


UTU ni kutambua ubinadamu wetu na kutenda kwa ufahamu.


UPENDO bila sababu ni msingi wa Uumbaji na nguzo ya mahusiano yoyote.


UMOJA ni uelewa kwamba wote ni sehemu ya mfumo hai uliyounganishwa na unaotegemeana!


Jumuiya yetu ilianzishwa kwenye mtandao wa FACEBOOK mwaka 2020 kwa malengo ya kusaidiana kutambua zawadi zetu na kuishi maisha yenye furaha yanayogusa jamii zetu. Ili kugeuza changamoto kuwa fursa, tuliamua kuwa na malengo manne yaliyo kwenye uwezo wetu na tunapeana moyo kwa HALI NA MALI kama ilivyokuwa Asili ya mababu zetu. #Ubuntu.